Mkuu wa wilaya ya Iramba Mkoani Singida Mhe: Emmanuel Luhahula amekabidhiwa madawati 225 kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo katika Mgodi wa Sekenke Nkonkilangi Wilaya ya Iramba kwa ajili ya shule za sekondari na misingi wilayani Iramba ili kuunga mkono jitihada za serikali.
Akizungumza na wachimbaji wadogo katika machimbo ya Sekenke yaliyopo katika Kijiji cha Nkonkilanga, Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui, Wilayani Iramba, Mkuu wa Wilaya ya Iramba amewashukuru sana kwa ushirikiano wao na kwa kujitoa kuchangia madawati.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Iramba amewaomba wachimbaji wadogo wadogo kuifadhi na kutunza mazingira ili yawe mazuri kwa lengo la kuepukana na Magonjwa ya milipuko.
Makundi ya wachimbaji waliochangia madawati ni Sekenke One Madawati 30, Iramba Nkulu Madawati 65, Iramba Kenkang’ombe Madawati 20, Uwema-Mzizini Madawati 10, Malaki-Uwaseke Madawati 20, Nassoro Plant Madawati 50, Maulid Plant Madawati 10 na Waziri Illution Madawati 20.
Vile vile Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa wale ambao wanawaomba Rushwa. “Suala la Rushwa halina mjadala, Rushwa ni adui wa haki, usikubali kununua haki yako, wananchi mnaombwa Rushwa lakini hamtoi taarifa, wananchi toa taarifa ili tuwakamate hao waarifu” alisema Mhe Luhahula
Afisa TAKUKURU wilaya ya Iramba Ndugu Benjamin Masyaga alisema Rushwa ni tatizo ambalo athari zake zinamgusa kila mwananchi. Tatizo hili linasababisha jamii kukosa imani na Serikali yao, amani baina ya wanajamii, kujenga matabaka ya walionacho na wasiokuwa nacho. Vilevile rushwa imekuwa chanzo cha kudhoofisha huduma zinazotolewa katika jamii. “kila mwananchi sehemu alipo aweze kushiriki kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa bila kuchukua muda mrefu. Kila mwananchi anawajibika kuzuia vitendo vya rushwa na kutoa taarifa hizo ili kuchukuliwa hatua stahili za kisheria dhidi ya wala Rushwa na kutokomeza Rushwa nchini.
Ametoa wito wa kukataa kujihusisha na vitendo vya Rushwa ikiwemo kutoa au kupokea Rushwa na kuhakikisha wanatoa taarifa za vitendo vya Rushwa katika ofisi za TAKUKURU zilizo wilayani Iramba au kwa kupiga simu ya bure namba 113 au kwa vyombo vingine vya dola na viongozi wanaohusika.
Ameongeza kusema wananchi watoe ushirikiano kwa TAKUKURU na vyombo vingine vya dola na kuwa tayari kutoa ushahidi wa vitendo vya Rushwa kwakuwa mara nyingi TAKUKURU imekuwa ikishindwa kufikia malengo kutokana na wananchi kutotaka kutoa ushirikiano
Mkurugenzi wa uhamiaji wilayani Iramba Ndg. Doto Selesini amewataka wananchi wa wilaya ya Iramba kutoa taarifa wanapobaini uwepo wa wahamiaji haramu ili kuthibiti raia wa kigeni na yeyote atayebainika kuficha wahamiaji haramu kwenye eneo lake atachukuliwa hatua kali za kisheria. Alitoa wito huo kwa wananchi kutowahifadhi wahamiaji haramu kwenye makazi yao sambamba na kuwataka watoe taarifa kwenye vyombo vya dola pale wanapogudua kuna mgeni asiyeeleweka na wanamtilia mashaka kwenye makazi yao.
Picha za madawati yaliyopokelewa na mkuu wa wilaya Iramba
Madawati yaliyochangiwa na kikundi cha wachimbaji wadogo IRAMBA KENKANG'OMBE mgodi wa Sekenke jumla ya Madawati 20.
Madawati ya kikundi cha wachimbaji wadogo MAULID PLANT mgodi wa Sekenke jumla ya Madawati 10.
Madawati yaliyochangiwa na kikundi cha wachimbaji wadogo UWEMA MZIZINI katika mgodi wa Sekenke jumla ya Madawati 10.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.