BAADA ya Rais Dkt. John Magufuli kurejesha Kikokotoo cha zamani kwa mafao ya WATUMISHI WA UMMA nchini, wafanyakazi kupitia mashirikisho huru ya vyama wameendelea kuunga mkono agizo hilo kwa kufanya maandamano ya amani.
Shirikisho huru la vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Singida, leo limefanya maandamano ya amani ya kumpongeza Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuondoa tatizo la KIKOKOTOO ambacho kilisababisha watumishi wengi kukosa amani na utulivu mioyoni mwao.
Maandamano hayo yaliyoanzia ofisi za TUCTA mkoa zilizopo mtaa wa Mughanga na kupitia mtaa wa Boma road kisha kupokelewa katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Singida na Dkt. Rehema Nchimbi ambaye ndiye mkuu wa mkoa wa Singida akisindikizwa na viongozi mbalimbali wa Vyama na Serikali.
Katika risala ya watumishi hao iliyosomwa na Katibu wa TUCTA mkoa, Bw. Max Chaba, wafanyakazi hao wamepongeza hatua ya Mheshimiwa Rais Magufuli kurejesha kikokotoo cha zamani, hali waliyoieleza kuwa amesikiliza maombi yao na sasa amefuta machozi yaliyokuwa yakiwatoka kwa muda mrefu sana.
Katibu huyo wa TUCTA amesema kuwa, uamuzi wa Rais Magufuli umepokelewa kwa furaha sana na watumishi wote wa mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla.
“Uamuzi huu umerejesha hali na morali ya watumishi wa umma nchini katika kufanya kazi kwa nguvu zao zote. Hii inatokana na imani kwamba baada ya kustaafu kuna kitu ambacho watakipata chenye nafuu cha kumwezesha kujikimu yeye mwenyewe na familia yake” Bw. Max amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUCTA mkoa wa Singida, Bw. Emmanuel Misholi, amesema kikokotoo kilichotangazwa awali kilikuwa ni JENEZA lililoandaliwa kwa ajili ya watumishi wanaotarajiwa kustaafu.
“Kwa kweli Rais Magufuli ni kiongozi msikivu mno amesikia kilio chetu na kuchukua hatua stahiki. Binafsi nina furaha na amani moyoni haijawahi kutokea. Sisi kama watumishi wa umma, hatuna zawadi ya kumpa Dkt. Magufuli isipokuwa ni kuchapa kazi na kukidhi mahitaji ya Watanzania wote bila ubaguzi” amesema Misholi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi amempongeza Rais kwa uamuzi wa busara, huku akiwataka watumishi wa mkoa wa Singida kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuleta ufanisi.
Mkuu huyo wa mkoa wa Singida, amewataka watumishi wa umma mkoani hapa kutumia furaha yao na amani waliyoipata baada ya kikokotoo kufutwa, kuongeza bidii ya kazi mara dufu katika kuitumikia Serikali na Watanzania ikiwa ni kumshukuru Rais Magufuli kwa kusikia kilio chao hicho cha muda mrefu.
Aidha, Dkt. Nchimbi amewaagiza wakuu wote wa idara, vitengo na viongozi wengine mkoani Singida, waendelea kuwa karibu na watumishi walio chini yao, na tabia ya kukemea, kuwatishia, isiwepo ili kumfanya mfanyakazi kuwa na amani wakati wote awapo kazini.
“Wafanyakazi, jambo hili ambalo mmelitambua na kuja kulisherekea leo kwa maandamano ya amani kwa ajili ya kumpongeza na kulitolea shukrani kwa Mheshimiwa Rais Magufuli ni jambo kubwa sana kwa uhai na uhai endelevu wa utumishi wetu na matunda ya kazi zetu”
“Hakika hakukukuwa na namna nyingine yoyote ya kusema isipokuwa ni kutoka na kusema hongera mheshimiwa Rais asante sana kwa haya yote uliyotufanyia na hasa la kutuondolea tatizo hili la kikokotoo… hongera mheshimiwa Rais Magufuli”.
“Waheshimiwa sana wafanyakazi, mnahaki tena mnahaki sana ya kumpongeza Rais na hata mngeamua kushinda kutwa nzima hapa kwa kumpongeza Rais mnahaki, na msiishie hapa endeleeni kumpongeza popote pale, hata mkiwa kwenye madawati yenu endeleeni kumpongeza. Hili la kikokotoo hili, sio letu ni la familia zetu na taifa kwa ujumla” amesema Dkt. Nchimbi kwa furaha tele.
Awali akizungumza baada ya kupokelewa maandamano, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Bw. Juma Kilimba, aliwaomba watumishi wa umma kufanya kazi karibu zaidi na Serikali yao ili kuunga mkono utekelezaji wa sera za Chama Cha Mapinduzi.
Kanuni ya kikokotoo kipya kilichokuwa kinalipa asilimia 25 ya mafao ya watumishi, kililalamikiwa sana na kupingwa na wadau wengi nchini, hali iliyomlazimu Rais Magufuli kuingilia kati na kurejesha utaratibu wa zamani.
Maandamano haya yameaandaliwa na chama cha wafanyakazi TUCTA mkoa wa Singida kwa ushirikiano na vyama vya CWT, TUICO, TALGWU, TUGHE, RAAWU pamoja na TAMICO kwa lengo la kumshukuru na kumpongeza Rais Magufuli kwa uamuzi wake wa kufuta kikokotoo.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.