WAJASIRIAMALI IRAMBA WAPEWA WITO WA KUCHANGAMKIA ZABUNI ZA VYAKULA
Wajasiriamali Wilayani Iramba wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo huduma za zabuni za vyakula kwa taasisi za umma ili kukuza mitaji na kuinua uchumi wao.
Wito huo umetolewa Agosti 2,2025 na Bw. Jeremia Kahurananga kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Yusuph Mwenda, wakati akifunga mafunzo ya siku sita ya wajasiriamali yaliyoendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Star Entrepreneur General lenye makao makuu mkoani Morogoro.
“Niwapongeze wajasiriamali 283 kwa kujitokeza kupata mafunzo ya ufugaji wa kuku, utengenezaji wa batiki, upishi wa keki na vitafunwa mbalimbali. Hakika mafunzo haya yawe chachu ya mafanikio katika kukuza uchumi wenu binafsi na jamii kwa ujumla,” alisema Bw. Kahurananga.
Aidha, aliwataka wajasiriamali kutumia vyema jukwaa la Ufunguzi wa Msimu wa Kilimo litakalofanyika Novemba mwaka huu kwa kutangaza bidhaa zao ili kujipatia masoko mapya.
“Lazima tuhakikishe mafunzo haya yanatusaidia kukuza masoko ya bidhaa zetu. Wilaya tayari ipo kwenye maandalizi ya ufunguzi wa msimu mpya wa kilimo 2025/2026,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika la Star Entrepreneur General, Bw. Daniphord Kesaga, aliishauri Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kuandaa maonesho ya wajasiriamali angalau mara mbili au tatu kwa mwaka ili kuwaongezea fursa za masoko. Pia aliiomba Serikali kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wajasiriamali kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Naye Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Iramba, Bw. Omary Lanjui, alisema idara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kusaidia wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo yenye riba nafuu, ikiwemo mikopo ya asilimia 10% kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri, mikopo ya 7% inayotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, pamoja na mikopo ya kibiashara kutoka Benki ya NMB.
Mafunzo hayo yaliwashirikisha wajasiriamali 283 na yalifanyika kuanzia Julai 28 hadi Agosti 2, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mjini Kiomboi.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.