Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewaeleza wananchi kuwa ni wajibu wao viongozi kueleza yale ambayo serikali imeyafanya na kwa nini imeyafanya kwa ajili ya wananchi ambao inaowaongoza.
Mwenda alibainisha hayo leo Alhamisi Machi 31, 2022 punde baada ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata nne za Tarafa ya Kisiriri wilayani hapa akiwa na kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kamati ya Usalama wilaya kuelezea mafanikio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka mmoja.
“Ni wajibu wetu wa msingi kutekeleza maoni na matarajio ya wananchi ambayo ndio vipaombele vyao.” Alisema Mwenda
Aidha, aliongeza kuwa wananchi huelezea kuwa wanayoshida ya maji, barabara na umeme ambapo serikali huyafanyia kazi na hivyo kuwa wajibu wa serikali kurudi kwa wananchi kuwaeleza yale ambayo serikali imefanya na kwa nini imefanya.
“Ndugu zangu wananchi! serikali inayoongozwa na Rais Samia imetekeleza miradi mingi na yenye thamani ya mabilioni ambayo leo nimeikagua na sasa imenilazimu kuwaeleza yale ambayo Rais Samia ameyatekeleza kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).”
Baada ya kuelezea miradi ya afya, maji, elimu, barabara na umeme iliyotekelezwa katika kila kata na yenye tahamani ya mabilioni, Mwenda alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wananchi mambo ya msingi yaliyombele ya wananchi kwa sasa.
Aliwakumbusha wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vijana waliopata ajira za muda kwa ajili ya kukusanya na kuweka namba ili kukamilisha mfumo wa anwani za makazi.
Halikadhalika, aliwataka wananchi na viongozi kuanzia ngazi ya kijiji na wilaya kuendelea kujiandaa na sensa ya watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika ifikapo Augosti mwaka huu.
“Ndugu zangu tujiandae kwa ajili ya kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi, tutoe changamoto na kuhakikisha kuwa zile kamati zinakutana na kuweza kuibua changamoto za awali ili serikali izipatie ufumbuzi kwa lengo la kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi.”
Mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani, wananchi mbalimbali katika maeneo tofauti tofauti wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuwajali wananchi kuwaletea miradi katika kila sekta.
Akiongea na wananchi wa kijiji cha Tyegelo kata ya Kidaru wilayani Iramba Diwani wa kata hiyo, Philipo Manguli alisema kuwa wanakila sababu ya kumshukuru Rais samia kwa kuwaletea miradi ya kihistoria.
“Kwa kweli miradi hii ni yakihistoria katika nchi yetu, hivyo ndugu zangu wananchi ni wakati sasa tuunge mkono kwa dhati juhudi za Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anatekeleza vipaombele vyetu.” Alishukuru Manguli
Kwa upande wake mmoja wa wananchi wa kijiji cha Tyegelo kata ya Kidaru, Salumu Mohamed alimshukuru Rais Samia kwa sababu maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya yamekuwa mkombozi wa kupunguza vifo vilivyokuwa vikitokea kutokana na umbali wa Hospitali.
“Sasa hivi hatuna shida maana hapo awali tulikuwa tunaangaika sana na wengine kupoteza maisha kwa kukosa tiba mapema.”
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.