Wazazi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida wametakiwa kuhakikisha wanawapeleka Watoto wao kwenye Vituo vya kutolea huduma za Afya kwa wakati ili wapate chanjo dhidi ya magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Wito huo umetolewa Disemba 17, 2024 na Afisa Tarafa, Tarafa ya Kisiriri Bw. Oswald Leopord kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Suleiman Yusuph Mwenda wakati akizungumza katika uzinduzi wa Wiki ya Chanjo uliofanyika kwenye Zahanati ya Bomani.
Aidha Oswald ametoa rai kwa wazazi pamoja na walezi kuhakikisha watoto walio chini yao wamepata chanjo zinazotakiwa kwa wakati ili kuwakinga dhidi ya magonjwa hatari na kuachana na Imani potofu kuhusu chanjo.
"Nitoe rai kwa wazazi wote kuhakikisha watoto wote wanapata chanjo zinazotakiwa kwa wakati kama tunavyoelekezwa na wataalamu ili kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa hayo hatari kama vile Surua na Polio....zamani watu walikuwa wakipata matatizo kwa sababu ya kutochanja kwa sababu ya Imani potofu. Tuachane na imani potofu tuwapeleke watoto wapate chanjo." Alisema Oswald Leopord
Kwa upande wake kaimu Mganga mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Daniel Paul Nkingo amesema Lengo la uwepo ya wiki ya chanjo na mwezi wa matone ya Vitamini A ni kuendelea kukumbushana na kuhamasishana kuhusu umuhimu wa chanjo katika jamii, kuwa fatilia na kuwaibua watoto walioasi chanjo na ambao hawakupata chanjo tangu kuzaliwa kwa sababu zozote zile ili waweze kupata chanjo na kuwaepusha na magonjwa yote yanayozuilika kwa chanjo, kuwapatia matone ya nyongeza ya Vitamini A pamoja na upimaji wa hali za Lishe kwa watoto wenye umri wa miezi 6-59.
"Lengo ni kuwakinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko yanayoweza kuzuiliwa na chanjo. Na tunaendelea kutoa Elimu na kuwaibua ambao hawajapata chanjo na walioasi chanjo ili wapate chanjo, kwa kufanya hivyo tunaamini Jamii yetu itakuwa imekingwa." Alisema Daniel Nkingo
Naye Mratibu wa chanjo Wilaya ya Iramba Jackson Shango Shillah amesema kuanzia January 2023 Hadi Novemba 2024 jumla ya watoto 1918 wameasi chanjo na zoezi hili litahusisha kuhakikisha wamepata chanjo.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.