By Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jaffo ameupongeza Mkoa wa Singida kwa kuwa miongoni mwa mikoa mitano nchini kwenye zowezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.
Jaffo ameyasema hayo leo Jumatano Novemba 06, 2019 akiwa Mkoani Singida kukagua utekelezaji wa kanuni na taratibu za uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea Nchini.
Pia amewapongeza wakazi wa Mkoa wa Singida kwa kuhamasika kujitokeza kwa wingi kitakwimu katika zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga kura.
Akiongea katika ziara hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jaffo amesema uandikishaji wa Daftari la Kudumu ni moja ya hatua muhimu ya mchakato wa serikali za mitaa.
“ Katika zoezi la uandikishaji Singida ni miongoni mwa mikoa mitano iliyofanya vizuri, na kwa wagombea tayari mfululizo wa siku 7 tumekamilisha zoezi la kuchukuwa na kurudisha fomu na hatimaye kufanya teuzi za wenyeviti na wajumbe wa kamati za rufaa,” alisema Jaffo
Waziri Jaffo amezitaka kamati zote za rufaa nchini kuhakikisha wanasimamia haki na usawa kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo iliyopo bila ya kumuonea mtu yoyote wakati wa maamuzi.
“Azma yetu sote ni kuona uchaguzi huu unakwenda vizuri na unakamilika kwa lengo la kuunda mamlaka za serikali za mitaa ambazo zinajibu matatizo makubwa ya wananchi,” aliongeza Jaffo
Akibainisha umuhimu wa zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa, Jaffo amesema uchaguzi huo unatengeneza serikali za mitaa zilizo karibu na wananchi, ambapo Taifa likitoa ajenda zozote za maendeleo basi utekelezaji na msingi wa maendeleo unatoka chini.
Jaffo amewataka wananchi kufahamu kuwa kwa mujibu wa kanuni zilizopo, “Kamati ya Rufaa ya Wilaya” inayoundwa na Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) ambaye ndiye mwenyekiti na kusaidiwa na wajumbe wanne ambao ni watumishi wa sekta za umma kutoka wilaya zote ndani ya mkoa huku katibu wa kamati hiyo anatoka ndani ya sekta ya umma na ataruhusiwa kupiga kura.
“Mwenyekiti nendeni mkazingatie haki, sikilizeni rufaa na malalamiko yote yatakayotolewa mezani kutoka vyama vyote na watu wote kwa uhuru na upana wake bila kuingiliwa na mtu yoyote,” alisisitiza Jaffo
Akisisitiza mbele ya wajumbe wa kamati ya rufaa mkoani Sin gida Tanzania, Jaffo amewaambia wajumbe hao watende haki na wasiogope.
“Mmepewa rungu lisilokuwa na mashaka , tendeni haki msiogope, hakikisheni kila kitu kinanyooka, kama kuna mtu anastahili haki mpeni haki yake na kama kunakasoro zirekebisheni,” aliongeza Jaffo
Kufuatia mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa kuendelea nchini Waziri Jaffo amelitaka jeshi la Polisi kupitia makamanda wa mikoa kuendelea kusimamia utaratibu uliowekwa kwa misingi ya amani na kamwe mtu yoyote asijitokeze kuchafua mchakato wa uchaguzi unaoendelea kwa maslahi yake binafsi.
Akiongea katika ziara hiyo Mwenyekiti wa kamati ya Rufaa ya Wilaya ya Singida DC mkoani hapo, Wilson Shimo, amesema kuwa wamejipanga kusikiliza malalamiko na rufaa zote kwa haki na kurekebisha kwa mujibu wa kanuni zinazowaongoza na kuweka wazi kuwa mpaka jana walikuwa hawajapokea malalamiko yoyote.
Naye mjumbe wa kamati hiyo, Patrick Zamba amesema kuwa watajitahidi kutoa maamuzi sahihi kwa muda mwafaka kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Akiongea katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt, Rehema Nchimbi amesema siku njema daima huonekana asubuhi huku akibainisha kuwa hatua ya mkoa huo kupokea hati ya ushindi na kuwa miongoni mwa mikoa mitano bora ni ishara njema.
“Singida ni njema, tena ni njema na ni njema sana ! na asubuhi hii njema ndio itabeba mchana wote kuwa mwema zaidi, kwa hatua zote mpaka kukamilika kwa mchakato mzima wa uchaguzi huu muhimu,” alisema Nchimbi
.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.