Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba , leo Novemba 27, 2024, ameungana na wananchi wa jimbo lake katika zoezi la kupiga kura kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji.
Dkt. Nchemba amepiga kura katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Misigiri, Kata ya Ulemo, Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.
Akizungumza mara baada ya kupiga kura, aliwasihi wananchi kuhakikisha wanatumia haki yao ya msingi ya Kikatiba kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo.
"Uchaguzi huu ni wa haki na demokrasia. Tumeshuhudia zoezi likiendeshwa kwa uhuru kabisa. Naomba wananchi wote ambao bado hawajapiga kura wajitokeze kwa wingi kufanya hivyo, kwani ni haki yao ya msingi," alisema Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa uchaguzi ni fursa muhimu ya kuchagua viongozi wenye maono ya maendeleo na uwezo wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
"Nimetimiza wajibu wangu wa kupiga kura, na niwaombe wananchi kote nchini kufanya hivyo kwa maslahi makubwa ya Taifa letu," alisisitiza.
Dkt. Nchemba aliambatana na Mkewe Bi. Neema Ngure katika zoezi hilo la upigaji kura.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.