Na Hemedi Munga
tehama@2020.go.tz
Singida - Iramba. Waziri wa Fedha na Mipango ambaye ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi, Dkt. Mwingulu Nchemba amesikiliza wananchi na kutatua mgororo unaodaiwa kuibuka punde baada ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuweka mabango ya matangazo yanayokataza shughuli za kilimo,mifugo na alama za mipaka katika eneo hilo.
Dkt Nchemba ametatua mgogoro huo leo Jumamosi Novemba 13, 2021 wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Mpambaa Tarafa ya Shelui wilayani Iramba mkoa wa Singida.
Aliwafahamisha wananchi hao kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Suleiman Mwenda ameridhia kuwa eneo hilo ambalo wanalima na kuishi waendelee na huku ambako hakulimwi kubakie kuwa ni eneo la malisho ya mifugo na kupanda miti inayosimamiwa na Wakala wa Huduma wa Misitu Tanzania (TFS).
“Ni lazima ndugu zangu mlime kwa sababu kilimo ni uhai wa mwanadamu, hivyo serikali ya kijiji mjipange ili muhakikishe watu wote wanapata sehemu ya kulima” alisema Waziri Nchemba na kuongeza kuwa
“Hatuwezi kuuwa mradi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na pia hatuwezi kuuwa shughuli za ufugaji, hivyo upande waliopo wananchi utaendelea na shughuli za mifugo na kilimo huku shughuli za TFS zikiendelea upande wa pili kwa kupanda miti ambayo inamanufaa katika maisha yetu.”
Dtk Nchemba aliwaomba wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuligawa eneo hilo lenye ukubwa wa takribani hekari 9651 linalodaiwa kuibuwa mgogoro kuwa nusu liwe la kilimo na makazi huku lile la TFS litumike kwa ajili ya kupanda miti pamoja na malisho ya mifugo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda aliwahakikishia wananchi hao kuwa kila mmoja atapata eneo la kulima.
“Niwahakikishie kila mmoja atapata shamba la kulima na asijitokeze yoyote akadai kuwa eneo hili ni mali yake, ardhi hii kwa sasa itabaki kuwa ni mali ya kijiji mpaka pale tutakapokuja kuigawa kwa wananchi wote.” Alisisitiza Mwenda
Kwa upande wake Mhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani hapa, Shabani Nyamasangara aliwaomba wananchi hao wasitoe mabango hayo pamoja na alama za mipaka wakati wakiwa wanaandaa utaratibu wa kuja kuyatoa.
Akiongea na mwandishi wetu, mmoja wa wananchi waliofika katika utatuzi wa mgogoro huo, Mathius Imambo, amewataka wananchi wenzake kuridhika na maamuzi yaliotolewa, huku akiwasihi kudumisha amani, kuzingatia taratibu na sheria ili kujiepusha na migogoro isiyokuwa na tija katika kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Naye Anastazia Kitundu akamshukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Mwigulu Nchemba pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
“Niwashukuru sana kwa sababu tulikuwa hatuna pakukimbilia wakati tunawatoto na vikongwe tunaoishi nao hapa, Kwakweli Mungu awasaidie na kuwabariki sana katika maisha yenu ili mlitumikie Taifa hili kwa muda mrefu.” alishukuru Kitundu
Mgogoro uliotatuliwa ulidaiwa kuibuka baada ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuweka mabango yenye matangazo yanayokataza kuchoma moto misitu, kukata miti ovyo, kuhamisha mpaka wa msitu, kuingiza mifugo msituni, kutengeneza mkaa na kulima kwenye eneo la hifadhi.
Mwisho
Waziri wa Fedha na Mipango ambaye ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi, Dkt. Mwingulu Nchemba akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kushoto wakitembelea eneo lililodaiwa kuibuwa mgogoro kati ya Wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kijiji cha Mpambaa Tarafa ya Shelui wilayani Iramba mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Fedha na Mipango ambaye ni Mbunge wa jimbo la Iramba Magharibi, Dkt. Mwingulu Nchemba akiwataka wananchi kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda kwa namna ambavyo amejitahidi kuusikiliza mgogoro uliodaiwa kuwepo kati ya Wananchi na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kijiji cha Mpambaa Tarafa ya Shelui wilayani Iramba mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.