Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kwa kutokuwa na madeni yatokanayo na zao la pamba toka kwa wakulima walioko katika AMCOs ya Malendi na Shelui.
Waziri Hasunga ametoa pogenzi hizo leo agosti 10, 2020 wakati alipofanya ziara katika AMCOs ya Malendi na Shelui Wilayani hapa.
“ Nimefurahi sana kwa kuwa leo nimekuja kukagua pamba inayozalishwa na madeni kama wapo wanaodai hawajalipwa mwaka jana na kwa kuwa nyie hamna anaye dai ninawapongeza sana” amepongeza na kuongeza kuwa
“Ni wakati sasa wakulima wa pamba kuhakikisha wanalima pamba kisasa kwa kutumia mbegu bora ili waweze kupata kilo 1500 kwa hekari moja, hivyo mkulima ataona faida ya kilimo.”
Amefafanua kuwa mkulima atakapopata pamba yake Serikali haitaki kusikia mwanchi hajalipwa fedha zake, kila aliye lima pamba alipwe fedha zake kwa wakati ili nao wafurahie maisha.
“Ninaomba niwaambie Wakulima wenzangu kuwa pamba hii ndio inatuletea fedha za kigeni, ikachakatwe tuweze kupata nguo tunazo vaa, hivyo pamba ni zao la mkakati wa kitaifa ambayo tunataka kuhakikisha inalimwa na kwa ufanisi ili mkulima apate mavuno bora.” amesema Waziri
Amefafanua kuwa kilimo ndio maisha yetu kwa sababu kinatupatia chakula, fedha, kinatoa malighafi, kinatoa ajira na kinajenga uchumi.
“Limeni kwa wingi ili mle maisha maana hata vitabu vya dini vinasema na asiye fanya kazi na asile, hivyo kila mmoja lazima afanye kazi ikiwemo kilimo, ufugaji na uvuvi pindi inapowezekana.” amesisitiza Waziri
Akitoa taarifa fupi mbele ya Waziri huyo, Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo, Marietha Kasongo amesema kuwa Wilaya ya Iramba inalima mazao ya chakula ambayo ni mahindi, mpunga, mtama, uwele,viazi vitamu, muhogo, maharage na kunde, huku zao la alizeti, pamba, vitunguu, karanga na dengu kuwa zao la biashara.
Marietha amesema kuwa Iramba haitakuwa na njaa kwa sababu msimu wa kilimo 2018/2019 ilizalisha tani 154,791 ya mazao ya chakula na ziada ni tani 87,714 huku msimu wa 2019/2020 ilizalisha tani 224,334 na kuwa na ziada 156,847 na kufanya hali cha kula kuwa nzuri katika wilaya yetu.
Akiongea kuhusu kilimo cha pamba, Kasongo amesema kuwa kilimo hicho kinaendelea kuimarika kwa kuwa wakulima wanakipenda.
“Kupitia AMCOs imeweza kukusanya takribani Kg 2, 040, 490 zenye thamani ya takriban Tsh 2.4milioni kwa misimu wa 2018/2019 huku msimu wa 2019/2020 imekusanya Kg 5milioni” amebainisha Kasongo
Halikadhalika, ameishukuru kampuni ya Biosustaini kwa kununua pamba kwa Tsh 900 kwa kilo ambapo takribani Kg 134,920 zenye thamani ya takribani 121.4milioni zimelipwa.
Kwa upande wake mmoja wa wanachama wa AMCOs hiyo, Rubeni Kabila ametoa kero yake kwa Waziri huyo, kuwa kuna dawa wanazo nunua lakina zinashindwa kuua vidudu waliopo katika mmea wa pamba.
“Tunashindwa kunufaika na kilimo cha kisasa kutokana na uwepo wa kiua dudu licha yakuwa tunajitahidi kulima kitaalam pamoja na kutunza shamba vizuri lakini wadudu wanashambulia, hivyo tunaiomba Serikali kutusaidia kupata dawa inayofaa kuua vidudu.” ameomba kabila
Naye katibu wa AMCOs hiyo, Magulya Malendela amesema kuwa kupitia AMCOs ya Malendi wameweza kuchangia mifuko mitano ya simenti kwenye ujenzi wa zahanati ya kijiji na michango mingine kwenye sekondari ya Mgongo.
MWISHO
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula akimuonesha Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga zao la pamba wakati alipotembelea AMCOs ya malendi agosti 10, 2020. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akisalimiana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati alipotembelea AMCOs ya Malendi agosti 10, 2020. Picha na Hemedi Munga
Afisa Kilimo na Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Marietha Kasongo akisalimiana na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga wakati alipotembelea AMCOs ya Malendi agosti 10, 2020. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akikagua pamba iliyokusanywa na AMCOs ya Malendi wakati alipofanya ziara katika kijiji hicho agosti 10, 2020. Picha na Hemedi Munga
Afisa Kilimo na Ushirika, Marietha Kasongo kushoto na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula kulia wakimuongoza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga kukagua zao la pamba katika AMCOs zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakati alipofanya ziara agosti 10, 2020.Picha na Hemedi Munga
Zao la pamba AMCOs ya Malendi ikiwa tayari kwa ajili ya kuuzwa. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.