Waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt. Charles Tizeba amefanya ziara ya kizindua msimu wa ununuzi wa Pamba Kata ya Mtoa wilayani Iramba Mkoani Singida.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Dkt Charles Tizeba aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Emmanuel Luhahula, Kaimu Mkrugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Bi. Marietha Kasongo, Viongozi wa Mkoa wa Singida na Viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba wamefanya ziara hiyo katika vijiji vya Msansao na Mtoa.
Dkt. Tizeba ametangaza bei elekezi ya kununulia pamba msimu huu wa 2018/19 kuwa shilingi 1,130/= kwa kilo moja ya pamba mbegu. Akizungumza na wananchi Dkt Tizeba amesema, “Msimu huu, bei ya pamba ni shilingi 1,130/= kwa kilo moja. Hii ni kutokana na bei katika soko la dunia kuwa haziridhishi, na kwamba bado pamba yetu nyingi inauzwa nje ikiwa ghafi hali inayotufanya tuwe tegemezi kwenye suala la bei, lakini Serikali iko katika mchakato wa kuhamasisha maendeleo ya Viwanda vya nguo nchini hali hii itaboresha bei ya pamba nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Emmanuel Luhahula Aliongeza kusema kwamba, katika msimu huu wa kilmo cha pamba Pembejeo zote zimetolewa bure kwa wakulima wa pamba pia kuwahakikishia wakulima wa pamba kuanzia msimu ujao wa kilimo, wakulima watapatiwa pembejeo zote ambazo ni mbegu za kupanda, Bomba za Kunyunyizia wadudu, viuadudu na kamba za kupandia bure bila kulipia gharama yoyote.
Dkt Tizeba amewashauri wakulima wa pamba baada ya kuuza pamba fedha zao zilipwe kupitia akaunti za benki au kwa kutumia M-pesa, Airtel Money n.k ili kuwa na usalama wa fedha zao. Aliongeza kusema wakulima walipwe kwa wakati na kwa kuzingatia sheria za ununuzi wa pamba pamoja na usafi na ubora wa pamba. Dkt Tizeba alisema usafi na ubora wa pamba ni suala ambalo linapewa kipaumbele kikubwa kwa sababu uchafu kwenye pamba unaathiri ubora na sifa ya pamba katika soko la dunia.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.