Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mheshimiwa January Makamba, ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Mhe. Emmanuel Luhahula, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashari ya Wilaya ya Iramba Mwl.Linno Mwageni, Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Iramba na Wakuu wa Idara na Vitengo wamefanya ziara ya kukagua baadhi ya maeneo yanayohusisha miradi ya mazingira Wiliyani Iramba mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Makamba katika ziara yake Wilayani Iramba aliweza kudhuru katika maeneo ya Bwawa la Ushora lililopo Kata ya Urughu Tarafa ya Ndago pamoja na Kutembelea Ziwa la Kitangiri katika Kata ya Tulya, Tarafa ya Shelui wilaya ya Iramba.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mhe, Simion Tiyosera Diwani wa kata ya Urughu(CCM), akiongea kwa niamba ya wananchi wa Iramba ameomba Waziri Makamba kurejea mpaka wa kimahesabu kati ya ramani ya Mkoa wa Singida na Iliyokuwa Shinyanga. Hii itasaidia mmiliki wa rasilimali ya Ziwa ambaye ni Halmashauri ya wilaya ya Iramba na kutoa mwongozo shirikishi wa kutunza na kuendeleza rasilimali ya Ziwa kwa manufaa ya watanzania wote na Wizara kusaidia Mpango wa Hifadhi ya Ziwa Kitangiri, na Bwawa la Ushora kwa ajili ya manufaa ya watanzania wa kizazi cha sasa na kinachokuja.
Mhe, Tiyosera aliongeza kusema, Ziwa Kitangiri lina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 105, takwimu za kisayansi na watafiti mbalimbali zinaonyesha kina cha maji kimepungua toka mita tisa (9) hadi chini ya mita sita (6) na kupungua kwa ukubwa wa Ziwa kwa zaidi ya 38% katika kipindi cha kuanzia mwaka 1972 hadi 2016.
Waziri Makamba amesisitiza Utashi, Utayari na Uwezo, Utunzaji mazingira na utunzaji wa Vyanzo vya Maji na Misitu katika maeneo ya jamii. “Maeneo ambayo tunaamua kuyaifadhi ni maeneo ambayo wananchi wenyewe wameamua tuyaifadhi. Tunapokubaliana eneo liifadhiwe, basi lazima kuwe na Utashi wa wananchi wenyewe, utayari na uwezo wao wa kuhakikisha wanalinda maeneo hayo na yanakuwa salama.”
Mhe. Makamba alisema kwamba Uhifadhi wa mazingira unahitaji wananchi wawetayari kujitoa na kuwa walinzi wao wenyewe na kushauriana na Serikali kwenda nao bega kwa bega kuhakikisha wanasaidiana katika utunzaji wa rasilimali hizo.
Ziwa kitangiri ni moja ya rasilimali muhimu, iliyopo katika Wilaya ya Iramba, ambalo linapakana na Wilaya ya Meatu kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, kishapu upande wa Mkoa wa Shinyanga na Igunga kwa upande wa Tabora. Shughuli mbalimbali za uvuvi zinazofanyika katika Ziwa hili zimekuwa zikitoa mchango mkubwa katika kuboresha lishe ya jamii na kukuza uchumi wa kipato cha kaya, kuboresha maisha na maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla na hatimaye kufikia kiwango cha uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Waziri Januari Makamba akisalimiana na wananchi wa Kata ya Urughu.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.