Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki amesikitishwa na kusimama kwa uzalishaji wa Kiwanda cha Yaza Investiment CO.LTD chenye uwekezaji wa takribani Tshs 10.2bilioni katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kupambana kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Kairuki ameyasema hayo leo Mei 29, 2020 wakati alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya uwekezaji katika kiwanda cha Yaza Investment CO. LTD kilichopo Tarafa ya Ndago Wilayani Iramba.
“Ni jambo ambalo halitii moyo kwa kiwanda chenye miundo mbinu yote, uwekezaji wa zaidi ya bilioni 10.2, kutoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 50 na zisizokua za moja kwa moja na manufaa mengine kwa watu zaidi ya 1000,” amesema Kairuki
Inadaiwa kuwa muda wa urejeshaji wa mkopo umekuwa ni mchache kwa uwekezaji mkubwa kama huu.
“Mkopo mkubwa kulipwa ndani ya mwaka mmoja, muda wa urejeshaji wa mkopo kwa swala la uwekezaji mkubwa umekuwa ni mdogo sana,” amesema Waziri
Halikadhalika, amemwambia Muwekezaji huyo, kuwa anayonafasi ya kuliwasilisha swala hili mahakamani kwa lengo la kupata tafsiri ya mkataba kuhusiana na mkopo alioupata toka benki ya NMB.
“Unayo nafasi kulipeleka swala hili mahakamani ili watafsiri mkataba kuhusiana na mkopo huu kuwa ulitaka nini, hatua ipi imekwenda sawa, ipi haijakwenda sawa na tunatokaje hapa tulipo,” amesema Kairuki na kuongeza
“Kuna haja ya Benki Kuu kufanya uchunguzi wa kina kwa namna ambavyo NMB walivyoliendesha swala hili, usimamizi walioufanya dhidi ya kiwanda hichi.”
Kwa kutumia kitengo cha usimamizi wa mabenki toka Benki Kuu Tanzania wanaouwezo wakujua wapi dosari ilitokea na kulitatua hilo kwa hatua za kibenki.
“Ni lazima Benki Kuu iliangalie swala hili kwa makini hatua kwa hatua kuanzia utoaji wa mkopo, nini hakikwenda sawa hata kama Muwekezaji katika maeneo mengine alikua na mapungufu lakini kama na nyinyi benki kuna maeneo mengine hamkuwa sawa nilazima hatua stahiki zichukuliwe,” ametilia mkazo Waziri
Akibainisha lengo kuu la ziara hiyo katika kiwanda hicho, Waziri huyo amesema kuwa ni kuangalia kiwanda hicho kinarudisha uwekezaji huku akiahidi kukaa na Muwekezaji huyo, NMB pamoja na Benki kuu ili kuona namna ya kutoka hapo kilipo.
Mapema akiwasilisha taarifa fupi ya uwekezaji wa kiwanda hicho namna kilivyosimamisha uzalishaji, Mkurugenzi Mtendaji, Yusuph Nalompa amesema kuwa mwaka 2012 waliomba mkopo wa uwekezaji wa Tsh 2bilioni benki ya NMB kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda.
Mwaka 2013 benki ya NMB iliikopesha kampuni hiyo Tsh 900milioni ambapo Aprili 15, 2013 ilitoa Tsh 460milioni mkopo wa muda mrefu wa mwaka mmoja huku Tsh 440milioni zikiwa ni overdraft.
Amefafanua kuwa fedha hizo za awali zilikuwa zikigawanywa kati ya benki na kampuni.
“Mhe, Waziri fedha hizo zilikuwa zikitotewa kidogo, hivyo benki ilikua inachukua nusu ikiwa ni marejesho nasi tunachukua nusu kwa ajili ya kujenga kiwanda kwa sababu hiyo kiwanda kikachelewa kukamilika hadi 2017,” amefafanua Nalompa
Amesema benki hiyo iliendelea kuipa kampuni fedha kwa njia ya overdraft nakufika Tsh 5bilioni huku wakichukua marejesho ya riba toka kwenye kampuni hiyo takriban bilioni tatu, milioni miatatu na ishirini na saba (3,327,000,000).
Baada ya kiwanda kukamilika mwaka 2017 kampuni hiyo iliiomba benki ya NMB mkopo wa kufanya biashara ambapo mei 18, 2018 NMB ilipitisha mkopa wa collateral manager ambao kampuni haikuomba.
Nalompa amesema mkopo huo ndio ulioua biashara kwa sababu ulikuwa unasimamiwa na benki kwa kuleta Afisa kiwandani alie simamia soko na kutoa taarifa NMB pale mkulima anapoleta alizeti kiwandani ndipo inatoa fedha ndani ya muda wa siku 3 au 4 baada ya kiao chao kupitia akaunti iliyoianzisha na kuisimamia yenyewe huku kampuni ikiwa haina uwezo wakutoa fedha katika akaunti hiyo.
Halikadhalika, amefafanua kuwa kampuni ilikua hairuhusiwi kuuza bidhaa mpaka watafute mteja alipe fedha kwenye akaunti inayosimamiwa na NMB ndipo NMB itoe kibali cha kutoa bidhaa hiyo, hivyo kampuni haikuwahi kupata mteja kutokana na ukawiaji huo.
Katika jitihada za kujikwamua na hali hiyo, Nalompa amesema alionana na Mkuu wa kitengo cha mikopa cha benk hiyo Agasti 20, 2018 Ndugu Mbogozi ambapo alituma maafisa wake kwenda kiwandani kufanya tathimini upya.
“Mhe, Waziri Oktoba 4, 2018 walifika maafisa toka benki hiyo nakusema wao ni benki ya biashara, hivyo tutafute benki zinahusu kilimo kisha tuwaunganishe nao ili waungane na kuweza kupata udhamini wakupata mkopo ili kuendelea na biashara,” amesema Nalompa
Ndipo nilipoifahamisha nakuomba mkopo benki ya wakulima TADB na wakawa tayari kutoa mkopa kwa sharti la kupata barua kutoka NMB ya udhamini wa kushirikiana ili kuiwezesha kampuni kapata mkopo.
Hata hivyo NMB waliitaka benki hiyo kulinunua deni la kampuni hiyo ambapo TADB hawakua tayari kufanya hivyo na kuamua kusitisha mchakato wa kuikopesha kampuni hiyo.
Kwa changamoto hiyo imefanya deni kufikia 5bilioni kutokana na riba nahivyo kusababisha uzalishaji kusimama.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi amemtaka Mkurugenzi wa kiwanda hicho atakapokutana na Waziri huyo Juni 01, mwaka huu kusema ukweli utakaosaidia kutoka hapa kiliponasa.
“Ndugu yangu Yaza hii ni fusra kubwa itumie ili kukihuisha kiwanda hiki nakutimiza azma ya kuifanya Singida iendelee kuwa Singida ya viwanda na inayokimbia kuelekea uchumi wakati,” amesema Mkuu wa Mkoa nakuongeza
“Kuitoa Singida kwenye umasikini, sifa ya njaa na ukame moja ya mbinu na nyezo ni kiwanda hiki.”
Naye Mkazi mmoja wa jirani ya kiwanda hicho, Betha Samson amemshukuru Waziri Huyo kuja kiwandani hapo ili Serikali iwasaidie kiweze kurejesha uzalishaji ili waweze kupata mafuta na kukuza uchumi wao.
MWISHO
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi akimtaka Mkurugenzi wa Kiwanda cha Yaza Investment kueleza umkweli pindi atakapo kutana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu juni 01, mwaka huu ili kufufua kiwanda hicho kianze uzalishaji. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Yaza Investment akimueleza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki sababu zilizopelekea kiwanda hicho kusimamisha uzalishaji. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki akielekea kukagua kiwanda cha Yaza Investment akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alioko kushoto kwa Waziri huyo na kuliani mwake ni Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Emmanuel Luhahula. Picha na Hemedi Munga
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni akijitambulisha kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Wiziri Mkuu, Angellah Kairuki. Picha na Hemedi Munga
Afisa biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Prosper Banzi akijitambulisha kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi alipotembelea kiwanda cha Yaza Investment Tarafa ya Ndago Wilayani Iramba. Picha na Hemedi Munga
Kiwanda cha Yaza Investment kilichopo Tarafa ya Ndago Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Angellah Kairuki akiaga hadhira iliyohudhiria wakati alipotembelea kiwanda cha Yaza Investment kilichopo Tarafa ya Ndago Wilayani Iramba Mkoa wa Singida. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.