Na Hemedi Munga
Singida - Iramba. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu amewaahidi wakazi wa kijiji cha Tintigulu kujenga daraja mto Kinshoka ili kupunguza adha ya kupata huduma za afya pindi mvua zinapokuwa zinanyesha na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kwa baadhi ya nyakati.
Waziri Ummy ametoa ahadi wakati alipofanya ziara ya kufungua ujenzi wa barabara yenye kilometa 7.3 kutoka Shelui mpaka kijiji cha Tintigulu wilayani Iramba Mkoa wa Singida.
“Ndugu zangu ingependeza sana kama tungeanza kujenga daraja kisha ujenzi wa barabara ukafuata.” Amesema waziri huyo na kuongeza kuwa
“Mhe, Rais amedhamiria kufungua barabara za vijijini na mijini ndio sababu kwa Wilaya ya Iramba imetengewa Tsh 7.3 bilioni kwa mwaka wa fedha ukilinganisha na bajeti ya mwaka jana ambapo ilitengewa takribani milioni mia nane (800,000,000). Hivyo kipaombele cha daraja ni muhimu sana.”
Akiwasilisha taarifa fupi kwa Waziri huyo Meneja wa TARURA Wilayani hapo, Mhandisi Evance Kibona amesema kuwa ujenzi huo utahusisha kusafisha eneo la barabara ukubwa wa hekta 8.78, kutengeneza tuta la barabara kilometa 7.3, kuweka changarawe kwa ujazo wa eneo ( ) 7665, kujenga karavati lenye milango 3 yenye upana wa mita 4.5 kilometa 3, kujenga makaravati 14 yenye upana wa mita 2 kilometa 1.5 na kujenga kivuko (drift) chenye ukubwa wa mita 27 kwa mita 5.
Amebainisha kuwa kumalizika kwa barabara hii kutasaidia kufungua mawasiliano na shughuli za uchumi katika vijiji 6 vilivyopo kati ya kata ya Shelui na Ntwike vyenye jumla ya wakazi 14,933 wilayani hapo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Tintigulu Wilayani hapo, Nkeno Nkamba amemshuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa sababu amewaletea fedha za kutengeneza barabara hiyo, wakiamini kuwa barabara hiyo itawasaidia kupita kwa urahisi kuja kituo cha afya kilichopo Shelui ambapo ni takribani kilometa 7.3.
Naye Elipendo Jumanne mkazi wa kijiji cha Tintigulu ameiomba serikali kuikamilisha barabara hiyo kwa haraka ili iwe rahisi kupata huduma za afya hasa wakati wa kujifungua.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.