Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida Innocent S Msengi; Amezindua rasmi Zahanati ya Kijiji cha Tutu Kata ya Kiomboi Tarafa ya Kisiriri Wilayani Iramba Zahanati ambayo inakusudiwa kuhudumia wananchi wapatao 1004 katika Kijiji hicho Cha Tutu.
Aidha Msengi, Akiwahutubia wananchi waliojitokeza kwa wingi, kwa lengo la kushuhudia uzinduzi wa Zahanati hiyo amewataka wananchi hao kuhudhuria kikamilifu na Kupata matibabu katika Zahanati hiyo, kwani kwa sasa changamoto ya kufuata matibabu kwa mwendo mrefu Zahanati ya Bomani umeisha.
Msengi Amesema kuzinduliwa kwa Zahanati hiyo kutaondoa kabisa vifo vya akina Mama na watoto ambao walikuwa wanayapata wakati wanafuata Matibabu Bomani au Hospitali ya Wilaya.
Mwenyekiti huyo wa Halmashauri, Amesema kwa sasa vifo vya akina mama vitapungua kwa asilimia kubwa kutokana na kukamilika kwa Zahanati nyingi katika vijiji Wilayani Iramba, lakini pia pindi vituo vya Afya vya Mtoa, na Shelui vitakapokamilika vitafanya vifo vya mama na mtoto kuwa ni historia katika Wilaya ya Iramba.
Aidha Msengi amebainisha kuwa Mpaka sasa,Tayari Tsh. Bilioni 1.5 zimeletwa kumalizia Zahanati Mbalimbali Huku huduma Katika Kituo Cha Afya Shelui tayari zimeanza, na kuongeza kuwa tayari shilingi Milioni 250 zimeletwa Kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya Shati Ili kuhudumia wananchi wa eneo hilo.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba Daniel Paul amesema Zahanati ya Tutu imekamilika na tayari imepewa Vifaa tiba huku wahudumu wa Afya tayari amefika kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Aidha wananchi wa Kijiji hicho wameishukuru serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali kuhusiana na Afya zao na sasa wamepona kilio chao cha muda mrefu.
"Kituo hiki kimekuja kwenye muda muafaka tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia,Mbunge wetu Mwigulu na Diwani wetu kijana Omary hakika wametufanyia mazuri sana." Amesema Mkazi wa Tutu Noel Mpinga.
Uzinduzi wa huduma Katika Zahanati ya Tutu umefanyika Novemba 19,2024 na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Chama Tawala na Serikali akiwemo Diwani wa Kata ya Kiomboi Omari Hassani Omari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Jeremia Kahurananga, Afisa Tarafa ya Kisiriri Oswald Leopord, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Iramba na Timu ya uendeshaji wa Hospitali ( CHMT) pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Tutu.
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.