Na Hemedi Munga
tehama@irambadc.go.tz
Singida - Iramba. Mkuu wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Suleiman Mwenda amewahakikishia akinamama kuwa swala la kubeba ndoo za maji kichwani punde linafikia ukomo wilayani humo.
Mwenda amebainisha hayo leo Jumanne Machi 30, 2022 punde baada ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata nne za Tarafa ya Kinampanda na Shelui wilayani hapa akiwa na kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kamati ya Usalama wilaya kuelezea mafanikio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka mmoja.
Akiongea na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nselebwe Tarafa ya Shelui, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia alielekeza zaidi ya Tsh 25 bilioni kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji yanayotoka Jijini Mwanza katika ziwa Viktoria kupitia Wilayani Igunga Mkoa wa Tabora hadi katika Tarafa ya Shelui wilayani Iramba.
Hali hii inafikia ikiwa ni ahadi ya Rais Samia wakati anaingia katika uongozi kuwa moja ya mkakati wake ni kuhakikisha anawatua ndoo ya maji kichwani akinamama.
“Moja ya watu wanaoteseka sana kwa tatizo la uhaba wa maji ni akina mama ambao huamka alfajiri na kupanga foleni ya maji na bahati mbaya wengine kupata changamoto ya kukamatwa na wanyama wakali mfano wa fisi.” Alisikitika Mwenda
Aidha, aliongeza kuwa akinamama hao wamekuwa wakitembea umbali mrefu wakiwa wamebeba maji kichwani hali ambayo hupelekea uzuri wao kuchuja na kuwafanya waume zao kuanza kutafuta wasichana wadogo huku ikiwa chanzo cha wake zao kuwa na sura zilizokakamaa ni kubeba maji kichwani na kutembea umbali mrefu.
“Hali hii katika utawala wa Rais Samia imefikia kikomo, tena basi, imekwisha!”
Uhakika huo unakuja ikiwa ni mwaka mmoja wa Rais Samia akiwa madarakani na kufanikiwa kuleta miradi mikubwa ya maji katika Tarafa ya Shelui.
Alifafanua kuwa ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia aliisha elekeza fedha takribani Tsh 25 bilioni kwa ajili ya kuleta maji toka katika Ziwa Viktoria kupitia Tinde mkoani Shinyanga, Igunga mkoani Tabora hadi Tarafa ya Shelui wilayani Iramba mkoa wa Singida.
“Hiyo ndio Tanzania ambayo mama yetu na Rais wetu Samia anayoijenga kwa kutoa maji Mwanza kuyafikisha Shelui.”
Ni dhahiri kuwa akinamama watatumia maji toka Ziwa Viktoria na kuvinufaisha vijiji 9 vinavyopatikana Iramba ambavyo ni Nselembwe, Kibigiri, Kizonzo, Tyeme, Mgela, Masagi, Msai, Mtoa na Nkyala.
“Ni nani kama mama! Ni nani kama Rais Samia! hakuna hakuna hakuna.”
Uwepo wa maji hayo, utasaidia akina mama kuchota maji nyumbani na kuhakikisha katika mabafu yao maji yanatiririka na hivyo wanaweza kupata huduma ya kunywa maji na kuoga kila wanapohitajia kufanya hivyo.
Aliwakumbusha wananchi hao kuwa, wao wakiwa viongozi wanalazimika kuyasema haya ili kuonesha kazi kubwa anayoifanya Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Hivyo hapana budi wananchi wampe ushirikiano na na kumuunga mkono Rais na kumuombea dua kwa Mungu ampe afya njema na weledi wa kuliongoza Taifa hili.
Akiongea katika hadhara hiyo meneja wa mamlaka ya maji vijiji na mjini Iramba, Ezra Mwacha alisema kuwa miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa katika tarafa hiyo na wilaya kwa ujumla ipo katika hatua ya ukamilishaji ili wananchi waweze kunufaika kwa kujipatia maji safi na salama.
Kwa upande wake mmoja wa akinamama aliyeonesha kiu ya kumuona Rais Samia na kumpongeza, Anna Lameck alisema kuwa ni kwa vile tu hawawezi kumuona Rais Samia kwa ukaribu ana kwa ana wangeweza kumpa zawadi kubwa kwa sababu amewatua ndoo kichwani.
Anna alisema kuwa wanamshukuru sana Rais Samia kwa kuwapenda akinamama na kuwajali kuwaletea maji karibu kwani imepunguza kwa kiasi kikubwa kasi ya wao kuacha uzingizi wao na kwenda kutafuta maji umbali mrefu.
Naye Robert Petro mkazi wa kijiji cha Wembere Tarafa ya Shelui alisema kuwa akinamama sasa hawapati tabu kama waliyokuwa wanaipata hapo zamani kwa sababu walikuwa wanakwenda kutafuta maji umbali mrefu na hivyo kujikuta wapweka katika baadhi ya nyakati hasa nyakati za alfajiri.
MWISHO
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.