Hemedi Munga, Irambadc
Iramba. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Linno Mwageni ametoa ombi kwa wataalam wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine walioendesha utafiti wa Mchango wa Kilimo – biashara Alizeti kuboresha maisha ya wakulima wanapopata nafasi nyingine kuwahusisha watoa maamuzi wengi wasikie mrejesho huu utakao wasaidia kupanga sera na kujua namna ya kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
Linno ameyasema hayo katika warsha ya mrejesho kwa wadau iliyofanyika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba, leo septemba 17, 2019.
Utafiti wa sera za kilimo barani Afrika unaozaminiwa na Shirika la Msaada la Maendeleo la serikali ya Uingereza (DFID) unaweza kuwa ni jibu la tulikuwa wapi, tuko wapi na wapi tunakwenda kwa wananchi wengi ambao tunaishi kwa kutegemea kilimo. Alisema Linno
Aidha amewataka watafiti kutumia utafiti wao kuwafikia wale ambao wamemaliza Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine ambao wanasema hawana ajira huku ardhi ipo, kufanya hivyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kujiajiri. Aliongeza Linno
Amewaagiza wakulima kutumia nafasi hii kutafuta haki zao ili watendewe inavyotakiwa kwa kuhakikisha wanawatumia maafisa ugani kikamilifu kwa kuwataka wawaoneshe mashamba yenye udongo unaofaa, mbegu inayofaa na kufuata kalenda kwa kila wanachotaka kukifanya kwa kufuata mpango kazi wa kilimo katika msimu husika. Alisema Linno
Akiwasilisha mrejesho kwa wadau wa matokeo ya utafiti wa majadiliano ya vikundi, Dkt, Kizito Mwajombe, amesema alizeti kama zao la kimkakati, kumekuwa na ongezeko la kilimo cha alizeti, hali hii imewavutia wawakezaji kujenga viwanda vikubwa ili kuchakata alizeti na hivyo kupanua wigo wa soko.
Huku akibainisha kuwa ongezeko la viwanda limechochea wakulima kuongeza uzalishaji wa alizeti na kupanua mashamba ekari 5 hadi 25 kwa kaya huku wakulima wadogo hekari 2 hadi 5, wakulima wakati hekari 6 hadi 10 na wakulima wakubwa hekari 11 hadi 50.
Aidha Dkt, Mwajombe ameeleza kuwa kilimo cha alizeti kinakabiliwa na changamoto ya kupungua kwa ardhi, ardhi kupungua rutuba, mbinu hafifu za utunzaji mazao baada ya mavuno na hivyo kusababisha kupungua ubora wa alizeti, bei kubwa ya mbegu bora ya alizeti, uhaba wa pembe jeo ngazi ya vijiji na bei ndogo katika uuzaji wa alizeti.
Naye Prof, wa Uchumi Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Aida Isinika, amesema kuwa wakulima wengi wa alizeti hawatumii teknolojia itakayo wawezesha kupanda vizuri kati ya shimo moja na jingine badala yake wanapanda kwa kurushia rushia.
Hata hivyo amewashauri maafisa Ugani kufanya semina elekezi kwa makundi mfano wakulima akina mama au baba watakaoweza kuwafundisha wenzao, kufanya hivyo kutasaidia matokeo ya alizeti kuwa makubwa.
Akiongea katika warsha ya wadau Mwenyekiti wa Chama cha Wasindika Alizeti Tanzania, Ringo Irigo amewataka wakulima kutochanganya mbegu bora za alizeti na zile zisizokuwa bora wakati wa uuzaji , huku akiwataka kufahamu kuwa Alizeti ni moja ya mazao ya kimkakati katika ujenzi wa uchumi wa viwanda Tanzania na nimoja ya mazao yanayopewa kipaombele katika mpango wa maendeleo ya kilimo.
Amewataka wakulima kujitambua kuwa ni watu muhimu sana katika uchumi wa nchi hii nakuwataka wabadilike walime alizeti kibiashara ili wapate faida na ikiwa ni jitihada za kuunga juhudi za serikali kuto agiza mafuta yakula nje ya nchi, kwa kuwa wakulima wanazalisha alizeti kwa wingi itakayotoa mafuta yakutosha nchini. Aliongeza Irigo
Akichangia mada mtendaji wa kijiji cha Nduguti Wilaya ya Mkalama, Johari Jumanne amewakumbusha viongozi kusimamia sheria ya vipimo vya alizeti wakati wa uuzaji, huku akiitaka serikali kutoa bei elekezi ya alizeti na kuwa na mfumo rasmi wa utoaji na upatikanaji wa taarifa za masoko bila kusahau kufikisha elimu kuanzia ngazi ya chini kuhusu matumizi sahihi ya mbegu bora na kilimo cha kisasa.
Akifunga warsha hiyo Dkt, Kashaga kutoka wizara ya kilimo amewataka wataalam, wakulima na wajasiriamali kafanyia kazi elimu itokanayo na utafiti wa matokeo ya utafiti wa majadiliano ya vikundi na ule wa matokeo ya utafiti wa dodoso katika kaya.
Utafiti ulifanyika katika wilaya ya Mkalama na Wilaya ya Iramba Mkoani Singida ambapo wilayani Mkalama umefanyika katika kijiji cha Dominiki, Nkalakala, Kisuluiga, Ndunguti, Mwanga, Lukomo na Isene huku kwa upande wa Iramba umefanyika katika kijiji cha Kidaru, Tyeme, Wembere , Luono, Ng’anguli, Mugundu, Mgungia na Zinzilingi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mwenye Suti akiwa na wataalam wa utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, nyuma ni wataalam mbalimbali baada ya warsha ya mrejesho wa mchango wa kilimo-biashara cha Alizeti kuboresha maisha ya wakulima wilaya ya Mkalama na Iramba. Picha na Hemedi Munga
Akichangia mada katika warsha ya mrejesho wa mchango wa kilimo-biashara cha Alizeti kuboresha maisha ya wakulima ukumbi wa Halmashauri wilayani Iramba, Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Mwampashe Zawadi. Picha na Hemedi Munga
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.