Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe. Emmanuel Luhahula amewaagiza watalaam wa lishe wilayani Iramba kuweka mkazo na kusimamia ipasavyo suala la lishe na kufanya wilaya ya Iramba kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwa na wakazi wenye afya bora.
Mhe: Luhahula amesema hayo leo wakati wa kikao cha kujadili suala la lishe Wilayani humo ambapo amesema suala la lishe duni limekuwa tatizo kubwa linalopelekea matatizo ya uwezo mdogo wa kufikiri, udumavu, utapia mlo, idadi ya watoto njiti, watoto wanaozaliwa na mgongo wazi, vichwa vikubwa, uono hafifu, ukosefu wa damu, vitamin na tatizo la ukondefu.
Aidha Mhe: Luhahula amesema wilaya Iramba imejidhatiti kukabiliana na tatizo la lishe kwa kutoa elimu ya lishe, kuzuia magonjwa ya upungufu wa viini lishe, kuongeza virutubisho kwenye chakula pamoja na matibabu ya utapiamlo.
"Maafisa lishe mnatakiwa kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia lishe bora ili kuondoa changamoto ya utapiamlo na udumavu katika jamii. maafisa lishe mnapaswa kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa kushirikiana na wadau kuhusu umuhimu wa lishe bora.
Kipaumbele lazima kiwekwe katika makundi maalum kama wazee, watoto, akinamama wanajawazito na wale wanaonyonyesha ili kufanikisha azma ya Serikali kuondoa Changamoto ya utapiamlo na udumavu"
Aidha aliwataka washiriki wa mkutano huo kuhakikisha kuwa kila mmoja anakuwa sehemu ya mapambano dhidi ya utapiamlo na udumavu hapa wilayani ili kujenga jamii yenye afya bora.
Akizungumza kwenye kikao, Mtalaamu Lishe kutokea OR-Tamisemi Ndug. Stephen Motambi amesema kuwa pasi na kuangalia mtoto amezaliwa kwa njia gani, ni muhimu kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi chote cha miezi sita ya mwanzo, bila kulishwa chakula kingine chochote.
“Mama anatakiwa amnyonyeshe mtoto wake ndani ya dakika thelathini mpaka saa moja baada ya kujifungua kama huyo mama amejifungua kwa njjia ya kawaida, na kama amejifungua kwa njia ya upasuaji baada ya saa tatu hadi nne anatakiwa awe ameanza kumnyonyesha mtoto” Amesema Motambi.
“ameongeza kusema kwa muda wa miezi sita mtoto anatakiwa anyonyeshwe maziwa ya mama pekee, asipewe chakula chochote kwani maziwa ya mama yana kila hitaji la mtoto katika umri ule hadi atakapotimiza miezi sita ya mwanzo, kuna faida za kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa kipindi hicho, faida hizo ni kwamba maziwa ya mama yanapatikana muda wote na hayana gharama, maziwa yanavirutubisho vya kutia nguvu, kutia joto, kujenga mwili na kulinda mwili, vilevile maziwa ya mama yana kiasi cha maji kulingana na umri na hitaji la mtoto, ni kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali, yanavirutubisho vinavyosaidia ukuaji wa mfumo wa fahamu wa mtoto, pia hujenga urafiki kati ya mama na mtoto na kingine unyonyeshaji hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya matiti na kizazi” Amesisitiza Ndgu Motamba.
Aidha Motambi ameeleza kuwa, kitaalam mtoto anatakiwa achanganyiwe vyakula vingine mbali na maziwa ya mama anapofikisha umri wa mizezi sita ya mwanzo tangu kuzaliwa, na kuongeza kuwa katika kipindi hicho vyakula anavyopaswa kupewa ni vile vitakavyoendelea kumsaidia katika ukuaji wake.
“Mtoto anapotimiza miezi sita ni kipindi ambacho unahitajika kumuongezea chakula cha ziada huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama mpaka miaka miwili au zaidi. Maziwa ya mama pekee hayatoshi kumpatia mtoto virutubisho vyote kwaajili ya ukuaji wake, pia mtoto huyu anakuwa ameshakuwa mkubwa kwa hiyo jinsi mtoto anavyokua ndivyo kiasi cha chakula kinatakiwa kiongezwe kufikia mahitaji yake ya lishe kwa ajili ya ukuaji zaidi”
“Vyakula ambavyo anatakiwa amtoto apewe kwa kipindi hiki, ni ule mchanganyiko wa makundi yote sita ya chakula, vyakula hivi ni Carbohydrate, hivi ni vyakula vya wanga vinavyotia nguvu mwilini- mfano uji wa nafaka kama Mahindi, Mtama, Mchele, Ngano, Viazi hili ni kundi moja, kundi jingine ni vyakula vya Protein hivi ni vyakula vya kujenga mwili kwa mfano Karanga, Maharage, Soya, Maziwa na Mayai”. Ameyataja makundi mengine kuwa ni…
“Kuna kundi la vyakula vya kutia nguvu na joto mwilini, kwa mfano mafuta ya mimea ikiwemo mafuta ya Kweme, mafuta ya Alizeti, Mzaituni, mafuta ya Nazi na mafuta ya kwenye maziwa pia mafuta ya Samaki. Kundi la nne ni Vitamin na kundi la tano ni Madini bapa huyu mtoto kwenye chakula chake anatakiwa aekewe mbogamboga na matunda, kama vile Karoti, Boga, Ndizi, Apple, na Matikiti na kundi la sita ni maji ambayo kwa kipindi chote tangu azaliwe mtoto huyo hajapewa maji, kwa hiyo baada ya kutimiza miezi sita anaweza kuanza kupewa maji kwa sababu mtoto huyu tumeshaanza kumchanganyia vyakula vingine”.
Ameongeza kuwa mchanganyiko huo wa vyakula ni muhimu pia iwapo utazingatiwa utaratibu unaoelekezwa na wataalam, utamuepusha mtoto na magonjwa kama ya utapiamlo kutokana na kukosekana kwa utaratibu mzuri wa lishe.
“Chakula kinatakiwa kiandaliwe katika mazingira safi na salama, kisiwe na vitu vigumu kama vifupa au mbegu mbegu, ni muhimu kutochanganya vyakula vingi kwa wakati mmoja kwa sababu mtoto anaweza kupata aleji ukashindwa kujua nini kimemsababishia hiyo aleji, kwa hiyo unatakiwa wakati unaanza kumlikiza huyu mtoto uwe unaanza chakula kimoja kimoja, kwa sababu mtoto huyu wa miezi sita pia anatakiwa anyonye kwanza kabla ya kupewa chakula cha ziada”Amesema Motambi
“Vyakula vya ziada anatakiwa apewe mara mbili au mara tatu kwa siku na visizidi vijiko vitatu vya chakula kwa siku, na vyakula vya mtoto vyote huwa vinachemshwa na havitiwi viungo vyovyote”.
Ameongeza kuwa “Mtoto wa miezi 7-8 anaweza kupewa mchanganyiko wa makundi yote ya chakula katika mchanganyiko uliopondwa baada ya kunyonya maziwa ya mama, ambapo anatakiwa apewe chakula cha ziada mara mbili hadi tatu kwa siku kwa idadi ya vijiko vitatu hadi tisa kwa siku. Pia mtoto wa miezi 8 anapenda kushika mwenyewe, hivyo unaweza kumpa vyakula vya kushika kama Maandazi, Chapati akawa anashika huku anakula mwenyewe” Amesema Motambi
“Kwa mtoto wa miezi 9-12 umri huu mtoto huwa na meno pia huwa anafahamu ladha ya chakula mbalimbali, hivyo unaweza kumlisha vipande vidogo vidogo vya chakula kigumu au vyakula laini vilivyopondwa, umri huu mtoto anaweza kupewa milo mitatu hadi minne ya chakula kwa siku.
Kama mtoto anaweza kula kwa mikono yake ni vizuri kumuacha pia kujizoesha kuchukua vitu na kula. Na umri wa miezi 12-24 yaani miaka miwili, umri huu mara nyingi mtoto anakuwa anatembea, anaanza kuongea na pengine wakati mwingine analazimisha hata kula mwenyewe, ni umri unaoweza kuanza kumpa vipande vidogo vya chakula hata vyakula vinavyoliwa na familia, na apewe milo mitatu mpaka mitano kwa siku” Amesema Motambi.
ameongeza kusema kuwa ulishaji mbovu wa mtoto usiozingatia maelekezo ya wataalam, kunaweza kusababisha udumavu wa mtoto kiakili na hata kimwili.
“Ulishaji mbaya wa mtoto ndio unatuletea watu sasa hivi, unaona vijana wengi unamwambia fanya hivi hafanyi, yani wapo tu kwenye kazi za kawaida kawaida, kwahiyo kama mama yake au familia yake ingeweza kumlisha vizuri kama inavyotakiwa huyu mtoto angekuwa vizuri na ndo zile A za darasani la kinyume chake ndo yale masifuri mengi ambayo sasa hivi tunahangaika nayo na mwisho tunapata viongozi wabovu na wenye maamuzi mabovu”.
Ndgu Motambi amesisitiza wazazi kuzingatia lishe zao katika siku elfu moja, kabla ya kupata ujauzito, kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua, akisema siku hizo ndio mustakabali wa mtoto katika maisha yake yote.
Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa Lishe, mratibu wa lishe mkoa wa Singida Bi. Teda Sinde amesema Lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo. Lishe duni pia hudumaza ukuaji wa watoto kimwili na kiakili hivyo kupunguza uwezo wa kufanya vizuri mashuleni pia hupunguza ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima, ndio maana msisitizo unawekwa kuwekeza Lishe bora katika siku 1000 za mwanzo za mtoto yaani kuanzia mimba inapotungwa mpaka mtoto anapotimiza miaka 2 ili kuondokana na tatizo hili la Udumavu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba Mwl. Linno Mwageni akizungumza kwenye kikao cha wadau wa lishe wilayani Iramba.
Mtalaam wa Uchumi kutoka OR-Tamisemi Ndgu. Hamza Mdoe akiwasilisha mada ya Maboresho kwenye Mfumo wa PlanRep Iliyoboreshwa katika kikao cha wadau wa lishe kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula
Mtalaam wa Lishe kutoka OR-Tamisemi Bi. Given Mlowe akiwasilisha mada ya Hali Ya Lishe Nchini katika kikao cha wadau wa lishe kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula.
Mratibu wa Lishe wilayani Iramba Bi. Monica Sarwat akiwasilisha mada ya Hali Ya Lishe wilayani Iramba katika kikao cha wadau wa lishe kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula.
Mdau wa Lishe Bi Jenipha Temu akichangia mada katika kikao cha lishe kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula
Washiriki wa kikao cha wadau wa lishe wakifuatilia majadiliano kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya ya Iramba Mhe: Emmanuel Luhahula
KIOMBOI, IRAMBA
Anuani ya Posta: P.O BOX 155. KIOMBOI-IRAMBA
Simu: 026 - 2532253
Simu: 026 - 2533001
Barua pepe: ded.irambadc@singida.go.tz
Copyright ©2017 Iramba District Council . All rights reserved.